Saturday, July 24, 2010

Muadhama ashtakiwa kwa kuendesha hospitali ya wenda wazimu

"...alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh50,000"

Na KHALWALE JAMES

KIONGOZI wa Kanisa aliyezua utata Muadhama John Juma Pesa I jana alishtakiwa katika mahakama ya Kisumu kwa kuendesha hospitali ya wenda wazimu bila ya kibali.
Kasisi Pesa I wa Kanisa la Holy Ghost Coptic Church of Africa alikabiliwa na mashtaka mawili kwamba mnamo Mei 25 mwaka huu katika kanisa lake mjini Kisumu, alishirikiana na wengine kuendesha hospitali ya wenda wazimu.
Hospitali hiyo inayoitwa St Philip Coptic Medical Centre, ilisemekana kuendeshwa bila ya kuwepo kwa leseni kutoka kwa bodi ya matibabu.
Pia mahakama iliambiwa kuwa siku hiyo, alipatikana katika hospitali hiyo akiwa na pakiti ya dawa aina ya Hartmanns Solution Ringer Lactate, ambayo ni mali ya Serikali.
Kiongozi huyo wa kanisa aliyewakilishwa na mawakili wa kampuni ya Ondezo, alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh50,000 hadi Juni 29, kesi itakaposikizwa.
Kasisi Pesa I alikaa zaidi ya saa mbili kwenye seli za polisi huku wafuasi wake wakimsubiri nje ya mahakama, kabla ya kuingizwa kwenye gari na kuondolewa haraka na watu wake.
Wilayani Makueni, jaribio la chifu kukamata washukiwa wa uuzaji bangi lilimtumbukia nyongo, alipovunjwa mkono.
Bw Julius Muange na manaibu wake Bw Maurice Kitwii na Bw Thaddeus Makumbi, walivamia nyumba ya washukiwa wa uuzaji bangi mjini Wote kulipozuka vurugu.
Huku akiwa na bendeji kwenye mkono uliovunjwa, Bw Muange alisema jana afisini mwake kwamba alisukumana na washukiwa hao walipokuwa wakijaribu kutoroka, kabla ya kuvunjwa mkono wa kushoto.
Hata hivyo, manaibu wake wawili walimuokoa kutoka kwa hasira za washukiwa hao. Walifanya msako ndani ya nyumba hiyo na kupata misokoto ya bangi na lita 300 za pombe aina ya 'karubu'.
"Walinizidia nguvu na kutaka kuniangusha chini. Lakini niliokolewa na manaibu wangu, ingawa walifanikiwa kunivunja mkono, " akasema Bw Mauange.
Baadaye alipelekwa katika hospitali ya wilaya ya Makueni alikotibiwa. Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Makueni akisubiri kupelekwa mahakamani.

Habari hii iliwahi kuchapishwa katika gazeti la ushirika la Nation, Taifa Leo, 29/05/2010 Saturday Page: 1